BREAKING NEWS

[5]

KUOKOKA NI NINI?

Na Ibrahim J. Nzunda .
Kama mwanaume akimwambia mwanamke akisema…“Unajua mimi nakupenda sana… tena nakupenda saana… Lakini sipo tayari kua bwana wako. Yaani sipo tayari kua mume wako”. Je, mtu huyo atakua anampenda kweli huyo mwanamke? Basi maana ya kuokoka inapatikana kwenye huu mfano. Kwa maana wengi wanamwamini Yesu kua ndie Mwokozi wao lakini hawataki kumkiri na kumkubari awe Bwana wao – (uvuguvugu).
MSINGI NA MAANA YA KUOKOKA
Ndugu zangu… bila kuficha imeandikwa “kama ukikiri kwa kinywa chako kwamba ‘Yesu ni Bwana’, na kuamini moyoni mwako kwamba Mungu alimfufua kutoka kwa wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini na hivyo kuhesabiwa haki, tena kwa kinywa mtu hukiri na hivyo kupata wokovu”. Na chini kidogo inasema “Kwa maana, Kila mtu atakayeliitia Jina la Bwana, ataokoka’’ na tena imefafanuliwa waziwazi kabisa kua “Tazama, wakati uliokubalika ndio huu. Tazama, siku ya wokovu ndiyo sasa”. Kwani baada ya Kristo, “mwandamu amewekewa kufa mara moja tu na baada ya kufa akabili hukumu”. (Warumi.10:8-13, 2wakorintho.6:1, waebrania.9:27)

Kuokoka ni kitendo cha wewe kukubali kubatizwa kwa Roho Mtakatifu kwa kumkiri Yesu Kristo kwa kinywa chako kua Bwana na Mwokozi wako, na hivyo unakua umetahiriwa kiroho na kuzaliwa upya (born again) kwa njia ya rohoni (warumi 2:28-29, 10:10,1petro 1:23). Kuokoka sii kwa dhehebu flani tuu, bali ni kwa wote na madhehebu yote. Lakini wengi sana ni wapagani, kwani “Mtu ye yote ambaye hana Roho wa Kristo, yeye si wa Kristo”. Kuokoka ni kukubali kua “mkristo”. Mkristo maana yake ni “mtu wa Kristo” yaani yule ambae Yesu ni “Bwana na Mwokozi” wake.

Kwahiyo nikisema “mimi nimeokoka”, vilevile ninakua namaanisha kwamba hapa duniani nimeokolewa kutoka katika utawala wa shetani/giza na kupewa utawala wa Mungu kwa kupewa Roho Mtakatifu, ambae ndie guarantee ya uzima wa milele. Kuokoka ni utimilifu wa imani yako kwa kupokea wokovu kwa kumuamini Bwana Yesu, kwani maana ya imani ni “kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni udhahiri wa mambo yasiyoonekana” (Waebrania.11:1)

Kuokoka ni kitendo cha wewe ku-sign kua mwana wa Mungu kwa kukubali kuwa mtakatifu kwa utakaso wa damu ya Yesu na Hivyo wewe kupewa Roho Mtakatifu ambae kwa huyu unapigwa mhuri katika roho yako kama garantii ya wewe kuepuka/kuokolewa na adhabu ya mauti ya milele ndani ya ziwa la moto wa milele. Kwamaana “bila ya utakatifu, hakuna atakae mwona Bwana”. (Waebrania 10:10, 12:14 Waefeso 1:13-14 na Wagalatia 3:26-29)”

KWA KINYWA CHAKO UNABATIZWA KWA ROHO MTAKATIFU
Kutumia mdomo ni muhimu kabisa kwasababu kuna sheria iliwekwa na Mungu kua “Mauti na uzima viko katika uwezo wa ulimi”. Kwahiyo kwa ulimi wako mwenyewe utapata uzima wa milele kwa kukikiri kwa kinywa chako kwamba ‘Yesu ni Bwana’. Vivyo hivyo, kwa kinywa chako unaweza kupata mauti ya milele kwa kumkana Kristo au kwa kiburi cha wewe kuto kukiri kua “Yesu ni Bwana” wakati ukiwa hai hapa duniani. (Mithali.18:21). Vile vile kwa mdomo Adam alidanganywa na hatimae vizazi vyote vikapata mauti. Basi tena kwa mdomo wako unapata wokovu pia. Yaani kama vile kosa la mtu mmoja (Adam) lilivyoleta hukumu kwa watu wote, vivyo hivyo pia kwa tendo la mtu mmoja (Yesu) la haki huleta kuhesabiwa haki kule kuletako uzima kwa wote (Warumi.5:12-19, 10:8-13)

UKISEMA ‘YESU NI BWANA’ LAZIMA UWE NA DHAMIRA YA KWELI
Wengi wanasema na tena wanaimba kila siku makanisani mwao kua “Yesu ni Bwana” lakini hawajatia nia mioyoni mwao. Na kwa watu kama hawa Mungu anasema “Watu hawa wananiheshimu kwa midomo yao, lakini mioyoni mwao wako mbali nami. Huniabudu bure”. Neno Bwana maana yake ni Lord ambayo pia ni “Owner”. Kwa hiyo ukisema “Yesu ni Bwana wangu”…inamaana Mungu anakumiliki, roho yako imezaliwa upya (born again), na mwili wako ni hekalu la Roho Mtakatifu na wala sio wako tena. Kwahiyo lazima awe Bwana, kwani “Kama vile ambavyo mwili pasipo roho umekufa, kadhalika nayo imani pasipo matendo imekufa (Marko.7:6-7, 1wakorintho.6:13-20, Yakobo 2:26)

KUONGOKA VS KUOKOKA
Kuongoka maana yake ni “kusilimu”. Ni kubadilisha mfumo/imani moja kwenda nyingine. Kwa mfano Mtume Paulo aliongoka kutoka dini ya kiyahudi na baadae kuokoka kwa kupewa Roho Mtakatifu. Lakini wanafunzi 11 wa Yesu wao hawakuongoka bali waliokoka kwa kujazwa na Roho Mtakatifu. Kwa hiyo mtu anaezaliwa kwenye familia ya kikristo yeye haongoki bali anachohitaji ni kuokoka. Kuongoka ni neno linalotoka na “ongoa” na maana yake ni “convert”. Lakini neno kuokoka (to be saved) ni kitenzi cha nomino “wokovu” ambayo ni “salvation”. (math:18:3,Maten.15:3-11,1tim.3:6)

KUBATIZWA KWA MAJI VS KWA ROHO
Watu wengi hubatizwa kwa Roho kwa kujazwa na Roho Mtakatifu hata bila ya kubatizwa kwa maji. Hii inatokea sana injili ikihubiriwa sehemu ambazo watu hawayajui makanisa wala hawajawahi kubatizwa kwa maji. Hata familia ya tajiri Kornelio pia ilikua hivyo. Hadi mtume Petro alishangaa akasema “Je, kuna mtu ye yote anayeweza kuzuia watu hawa wasibatizwe kwa maji? Wamempokea Roho Mtakatifu kama sisi tulivyompokea”.
Kubatizwa kwa maji ni kwa ajili ya toba, Vilevile ubatizo wa maji ambao kila kanisa hubatiza ni kwa ajili ya kukubali kua mwanfunzi na mfuasi wa injili ya Yesu kristo. Na huu ubatizo hata wale wenye Roho Mtakatifu hubatizwa (Yohana 3:5-6,math.3:11-17). Kwa hiyo kubatizwa kwetu kwa maji ni kwa ajili ya kuipokea injili na kua mwanafunzi wa Yesu. Na ndio maana Yohana mbatizaji alisema “Mimi nawabatiza kwa maji, lakini Yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu”
Kwa mfano imeandikwa “Siku hizo Yohana Mbatizaji alikuja akihubiri katika nyika ya Uyahudi, akisema, “Tubuni, kwa maana Ufalme wa Mbinguni u karibu”. Kwa hiyo yeyote aliyeikubali injili hii ya ufalme wa Mbinguni alikua mwanafunzi kwa kubatizwa kwa maji. Yesu (sinless) alibatizwa kwa Maji si kwa ajili ya kupewa Roho Mtakatifu (Yeye alizaliwa nae tayari), bali ilikua ni kwa ajili ya kuchukua injili ya “Ufalme wa Mbinguni/Mungu”. Injili ambayo Yohana aliihubiri kuandaa njia kwa ajili ya Bwana Yesu. Na baada ya Yesu kuichukua injili hii kwa kubatizwa kwa maji, “Tangu wakati huo, Yesu alianza kuhubiri akisema: “Tubuni, kwa maana Ufalme wa Mbinguni umekaribia” (math.3:2-17, 4:17)
Baada ya Yesu Kufa msalabani na Kufufuka tena, Roho Mtakatifu akamwagwa duniani, na Kwa njia hiyo ufalme wa Mbinguni ukawa umewasiri duniani. Kwa maana kila mwenye Roho Mtakatifu ana utawala/Ufalme wa Mungu. Na ndio maana pia Yesu alisema ‘‘Amin, amin nawaambia, kuna watu waliosimama hapa ambao hawataonja mauti kabla ya kuuona Ufalme wa Mungu ukija katika nguvu”(mark.9:1). Hapa Akina Peter, Mathayo, n.k. walikua wamesimama nae miaka 2000 iliyopita na ndio hao pamoja na wengine waliopokea ufalme wa Mungu/Roho Mtakatifu kabla ya kufa.

KWA WANAOPOTEA… KUOKOKA NI UPUUZI KWAO
Imeandikwa “ujumbe wa msalaba kwa wale wanaopotea ni upuzi, lakini kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu ya Mungu”. Na mahali pengine inasema “Mtu ambaye hana Roho wa Mungu hawezi kupokea mambo yatokayo kwa Roho wa Mungu, kwa kuwa ni upuzi kwake, naye hawezi kuyaelewa kwa sababu hayo yanaeleweka tu kwa jinsi ya rohoni”. Lakini ni kwa neema ya Mungu isiyopimika, hata wenye dhambi huielewa injili na hata kuamini na kupata wokovu kwa kujazwa na Roho Mtakatifu (1korith.2:14-31). Kwani “hata tulipokuwa wafu kwa ajili ya makosa yetu, alitufanya tuwe hai pamoja na Kristo Yesu, yaani, mmeokolewa kwa neema. Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani, wala hii si kwa matendo yenu mema...” (Waefeso.2:1-10). (wengi sana mnayo hii neema likini mioyo ni migumu)

DHAMBI ZA MAUTI VS ZISIZO ZA MAUTI
Kwa mkono wa Yohana, Roho Mtakatifu anafafanua kwa kusema “Kama mtu akimwona ndugu yake anatenda dhambi isiyo ya mauti, inampasa aombe, naye Mungu atampa uzima mtu huyo, yaani, kwa wale ambao dhambi yao si ya mauti. Iko dhambi ya mauti, sisemi kwamba utaomba kwa ajili ya hiyo. Jambo lo lote lisilo la haki ni dhambi, lakini iko dhambi isiyo ya mauti”. Kwa walio okoka na watakao okoka; JIEPUSHENI NA UZINZI/UASHERATI (James.1:14-15.2:10-11, 1John.5:16-17, Acts.15:23-29, 1corinth.6:18, Walawi.20, Ephes.5:5, colos.3:5, Hebrews.12:16-17).

TUFANYE NINI ILI TUOKOKE?
Yesu mwenyewe amesema “Je, kuna ye yote miongoni mwenu, ambaye mtoto wake akimwomba samaki, atampa nyoka badala ya samaki? Au mtoto akimwomba yai atampa ng’e? Basi ikiwa ninyi mlio waovu, mnajua kuwapa watoto wenu vitu vizuri, si zaidi sana Baba yenu wa mbinguni atawapa Roho Mtakatifu wale wamwombao?” Na kwa upole kabisa Roho Mtakatifu anasema “LEO, kama mtaisikia sauti Yake, MSIFANYE MIOYO YENU MIGUMU”. Yeyote asie na Mwanga analo Giza. Tumia mdomo wako sasa. Popote pale ulipo chukua dakika mbili. OMBA NA AMINI, ILI UOKOKE LEO.
ONYO! TAFADHALI USIOMBE SALA HII KAMA UNAMZAHA MOYONI MWAKO NA BADO UNAPENDA GIZA ILI USIJE UKAWA MWANA WA IBILISI MALA MBILI ZAIDI. LAZIMA UJIKANE MWENYEWE NA UAMINI KWELI.
OMBA HIVI; 
“Bwana Yesu ninakuhitaji. Ninakushukuru kwa vile ambavyo ulizifia dhambi zangu msalabani. Naamini kwamba Mungu alikufufua kutoka kwa wafu. Nakiri kua mimi ni mdhambi. Nisamehe dhambi zangu zote nilizozifanya Kwa kuwaza, kunena, na kutenda. Nisaidie kuzishinda dhambi zote. nipokee uwe Bwana na Mwokozi wangu. Nitakase kwa damu yako ya thamani na unibatize kwa Roho Mtakatifu. Nizae upya kwa Roho Mtakatifu ili niwe Mwana wa Mungu. Wewe ni Bwana wangu kuanzia sasa hata milele… Amen”.
Imeandikwa na Ibrahim J. Nzunda, Akiongozwa na Roho Mtakatifu
. [Pata softcopy. Tuma email yako kwenda 0754 210 627]
KUOKOKA NI NINI? KUOKOKA NI NINI? Reviewed by Unknown on 11:28 PM Rating: 5

Sora Templates