BREAKING NEWS

[5]

JE UTAFANYAJE, UKIMUONA RAFIKI YAKO WA KARIBU SANA, ANAELEKEA KATIKA ENEO LENYE HATARI KUBWA.?

Mfano unamwona rafiki yako kipenzi anaelekea katika eneo lililotegwa bomu hatari na unafahamu kwa hakika kuwa bomu hilo litalipuka baada ya muda mchache, nini utafanya ili kumsaidia rafiki yako?


Bila shaka jibu lako litakuwa ni kumpa taarifa juu ya hatari iliyopo mbele yake na kumzuia asiende katika eneo hilo. Lakini jaribu kutafakari kama rafiki yako atakataa kukusikiliza juu ya taarifa unayompa kuhusu hatari iliyo mbele yake utafanyaje?

Mfano huu unafanana sana na maisha tunayoishi wanadamu sasa. Watu wengi wanaelekea katika hatari kubwa( jehanamu) bila wao kufahamu wanaelekea katika hatari itakayowagarimu mateso ya milele.

Yawezekana ni kufungwa kwa fahamu zao juu ya hatari iliyo mbele yao au ni kiburi cha uzima kinachosababisha kila siku watu kupiga hatua kuelekea katika ziwa la moto. Neno la MUNGU linatufundisha kuwa baada ya kifo ni hukumu (waebrania9:27 Na kama vile watu wanavyowekewa kufa mara moja, na baada ya kufa ni hukumu;) Neno hukumu maana yake kutenga walio na haki na wakosefu watako elekea jehanamu.

Mwanadamu yoyote atendaye dhambi anamuasi MUNGU na mahali pake ni katika ziwa la moto (1yohana3:4 kila atendaye dhambi, afanya uasi; kwa kuwa dhambi ni uasi.)

Ni mara ngapi umemuasi MUNGU kwa njia zako zisizofaa lakini bado MUNGU amekuhurumia na kuendelea kukumbusha na kukusisitiza ili usiendelee kupiga hatua kuelekea hatarini (jahanamu)

Jaribu kufikiri, kama MUNGU angemhukumu mwanadamu kwa kifo kila akifanya kosa moja tu,ungekuwa wapi leo? Jehanamu au mbinguni katika uzima wa milele.

Endelea kujiuliza kuwa mbona pamoja na mabaya unayoendelea kuyafanya lakini bado MUNGU anakuacha ueendelee kuishi? Je unafikiri MUNGU haoni makosa unayoyafanya? HAPANA. Mungu anayaona makosa yako lakini anakupenda na anatamani ubadilike na ndio maana ujumbe huu uko mikono mwako ili akufundishe upate kutubu.( warumi5:8 Bali MUNGU aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi. Mstari huu una maana kuwa Kristo alishatufilia kwa ajili ya dhambi zetu naye anasubiri sisi tumkiri kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yetu ili atupe zawadi hiyo ya wokovu.

Yesu ndiye rafiki wa kweli, naye ameiona hatari iliyo mbele yetu na ndio maana aliutoa uhai wake ili tusiifikie hatari hiyo  (yohana3:16 Kwa maana jinsi hii MUNGU aliupenda ulimwengu , hata akamtoa mwanawe pekee, ili KILA MTU amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.) mstari huu unatuonesha kuwa nafasi ya kuokoka ni ya kila mmoja,na ndio maana unasema kila mtu (yeyote) amwaminiye asipotee.

Tena MUNGU bado anatuonya kuwa, yote tunayoyaona yanafaa na yanapendeza macho ni ya kitambo tu ( muda mfupi) nayo yatupeleka katika hatari kubwa ( jehanamu ) 1yohana2:15 msiipende dunia, wala mambo yaliyo katika dunia. Mtu akiipenda dunia kumpenda Baba hakumo ndani yake. 16 maana kila kiliichomo duniani, yaani tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia.17 Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu hata milele.
Kumbuka vitu vyote kwa mwanadamu havina uhakika, bali kifo peke yake ndio kitu chenye uhakika kwenye maisha ya kila mwanadamu.

Mfano huna uhakika kama utaweza kuoa au kuolewa, au kama utakuwepo baada ya saa moja lijalo au hutakuwepo,au kama baada ya dakika mbili macho yako yataendelea kuona au utakuwa kipofu BALI una uhakika wa asilimia mia moja kuwa siku moja Utakufa. Hii ina maana kwamba, inatupasa kujiandaa na kuwa tayari wakati wowote kuondoka duniani,(1petro4:2 Tangu sasa msiendelee kuishi katika tamaa za wanadamu, bali katika mapenzi ya MUNGU, wakati wenu uliobaki wa kukaa hapa duniani. 3a Maana wakati wa maisha yenu uliopita watosha kwa kutenda mapenzi ya mataifa;..)

Hujachelewa ndugu yangu, saa ya wokovu sio jana au kesho, bali ni sasa. MUNGU anatamani kila mtu afikirie toba na kuyaacha matendo yake maovu (1petro3:8 Lakini, wapenzi, msilisahau neno hili. Kwamba kwa Bwana siku moja ni kama miaka elfu, na miaka elfu ni kama siku moja 9. Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama wengine wanavyokudhani kukawia. Bali huvumilia kwenu, maana hapendi mtu yeyote apotee, bali wote wafikilie toba.). Yesu hapendi mtu yeyote apotee na kuelekea katika mateso ya milele jehanamu, ndio maana anaaendelea kukumbusha leo. MUNGU akusaidie uamue leo kuacha kuishi kwa kutazama vitu vya muda mfupi bali macho yako yatiwe nuru na uweze kuona upendo wa Yesu Kristo katika maisha yako.

MUNGU akuwezesha kuchukua maamuzi magumu ya kubadilika lakini yenye faida kwa maisha yako ya sasa na baada ya kifo (isaya48:18 Laiti ungalisikiliza amri zangu! Ndipo Amani yako ingalikuwa kama mto wa maji, na haki yako kama mawimbi ya bahari)

Je unayo sababu ya msingi kumzuia Yesu Kristo kuingia katika maisha yako leo? Kumbuka Yesu peke yake ndiye anayeweza kukuepusha na hatari iliyoko mbele yako (jehanamu). Kama uko tayari kumpokea sasa, sema sala hii kwa kumaanisha kutoka moyoni mwako;
Mungu Baba katika jina la Yesu, najua mimi ni mwenye dhambi, ninaomba unisamehe dhambi zangu zote, naamini Yesu ulikufa msalabani kwa ajili ya dhambi zangu na ukafufuka kutoka kwa wafu. Leo nimeamua kubadilika kutoka njia zangu zisizofaa na kukukaribisha Yesu moyoni mwangu na katika maisha yangu. Ninaamini na kukufuata wewe Yesu kama Bwana na mwokozi wa maisha yangu. Amen

Kama umesema sala hii kwa Imani basi Mungu amekusame dhambi zako zote na ndio umeanza uhusiano mpya na Mungu. Usiendelee kujihukumu bali songa mbele katika Imani(warumi10:13 kwa kuwa, kila atakayeliita jina la Bwana ataokoka.)
MUNGU AKUBARIKI NA AKUTETEE KATIKA HALI ZOTE.

If you were to die tonight and stand in front of God, and He asked “why should I let you into Heaven” what would you tell Him? Mark Cahill.

IMEANDALIWA NA ROHO MTAKATIFU KUPITIA JACKSON JOSTER CHELEJI.
EMAIL. jacksoncheleji@yahoo.com

JE UTAFANYAJE, UKIMUONA RAFIKI YAKO WA KARIBU SANA, ANAELEKEA KATIKA ENEO LENYE HATARI KUBWA.? JE UTAFANYAJE, UKIMUONA RAFIKI YAKO WA KARIBU SANA, ANAELEKEA KATIKA ENEO LENYE HATARI KUBWA.? Reviewed by Unknown on 4:43 PM Rating: 5

Sora Templates